LIPALE: OPARESHENI YA USALAMA BONDE LA KERIO INAENDELEZWA KWA UBAGUZI.

Mwenyekiti wa chama cha KUP kaunti ya Pokot magharibi Geofrey Lipale amekosoa jinsi ambavyo maafisa wa usalama wanaendesha oparesheni ya kukabili wahalifu wanaosababisha hali ya utovu wa usalama mipakani pa kaunti hiyo na kaunti jirani ya Elgeyo marakwet.

Lipale alidai kwamba oparesheni hiyo inaendeshwa kwa mapendeleo hali ambayo imepelekea kufungwa baadhi ya shule kwenye mipaka ya kaunti ya Pokot magharibi hali shughuli za masomo zinaendelea upande wa kaunti ya Elgeyo marakwet.

“Hii oparesheni ya usalama inayoendeshwa hasa kwenye mpaka wa kaunti hii na ya Elgeyo marakwet inaendeshwa kwa ubaguzi. Kwa sababu shule nne upande wa pokot zimefungwa huku zile za elgeyo marakwet ambazo zinapakana na kaunti hii zikiendeleza shughuli za masomo.” Alisema Lipale.

Lipale aidha amewasuta baadhi ya viongozi wa kaunti hiyo kwa kile alidai kwamba hawajafanya juhudi zozote kuhakikisha shule zilizofungwa maeneo hayo kufuatia utovu wa usalama zinafunguliwa na kuwaruhusu wanafunzi eneo hilo kuhudhuria masomo.

Mimi nawalaumu viongozi kaunti hii kwa sababu licha ya kuwa na nafasi, hawajafanya juhudi zozote kuhakikisha kwamba serikali inafungua shule hizo. Waziri wa usalama Kithure Kindiki alikuwa kaunti hii akiahidi kwamba shule hizo zitafunguli ila hadi kufikia sasa hamna hatua ambazo zimepigwa.” Alisema.

Lipale sasa anawataka wabunge katika bunge la kitaifa kutoka kaunti hii kuwa msitari wa mbele kutetea haki ya wanafunzi walioathirika akitishia kuongoza maandamano maeneo hayo iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa kushughulikia hali hiyo.

Ninawaambia wabunge katika bunge la taifa hasa kutoka kaunti hii kusisitiza swala la shule hizo kufunguliwa la sivyo mimi na wengine tutafanya mikutano na wakazi wa maeneo hayo na hata kuongoza maandamano hadi shughuli za masomo zirejelewe kwenye shule  hizo.” Alisema.