WAKAZI POKOT MAGHARIBI WAHIMIZWA KUPANDA MIMEA KANDO NA KILIMO CHA UFUGAJI.
Wito umetolewa kwa wakulima katika kaunti ya Pokot magharibi kukumbatia kilimo cha mimea mingine kando na shughuli za ufugaji ili kuhakikisha usalama wa chakula ikiwa moja ya ajenda kuu za serikali.
Akizungumza katika uzinduzi wa shughuli ya kupeana miche hasa ya miembe kwa wakulima eneo la Kacheliba, mshirikishi wa mradi wa Kenya climate smart agriculture Philip Ting’aa alisema kwamba hatua hiyo pia itaimarisha uwezo wa kimapato wa wakazi pamoja na kuhakikisha lishe bora miongoni mwa jamii.
“Tunataka wakazi kupanda pia mimea na kutotegemea tu ufugaji, ili waimarishe uwezo wao wa kifedha kupitia mazao ambayo yatatokana na mimea hiyo, na pia kuwa na lishe bora.” Alisema Ting’aa.
Alisema ipo haja ya wakulima kukumbatia kilimo cha mimea kutokana na changamoto ambazo huambatana na kilimo cha ufugaji ikiwemo ukame pamoja na wizi wa mifugo ambao mara nyingi hupelekea utovu wa usalama.
“Tunafahamu kwamba ufugaji huambatana na changamoto nyingi mfano ukame ambao unapelekea wengi kupoteza mifugo. Pia tatizo la utovu wa usalama huzungukia mifugo. Hivyo ili kukabiliana na hali hii wakazi wanapasa pia kujihusisha na upanzi wa mimea.” Alisema.
Waziri wa kilimo kaunti hiyo Wilfred Longronyang alisema kwamba miche hiyo iligharimu shilingi alfu 200 huku akitoa wito kwa wakazi ambao walinufaika nayo kuhakikisha kwamba wanaitunza vyema ili inawiri na kuwa ya manufaa.
“Nawaomba wakulima kwamba watunze vyema miche hii. Ikifika shambani isikae kwenye boma bali wapande na kuhakikisha kwamba wanainyunyizia maji ili ije kuwasaidia baadaye ikikomaa.” Alisema Longronyang.