MAKUNDI YA WAKULIMA 67 KUTOKA WADI TATU POKOT MAGHARIBI YANUFAIKA NA MBUZI AINA YA GALA KATIKA JUHUDI ZA KUIMARISHA KILIMO CHA UFUGAJI.

Mradi wa Kenya climate smart Agriculture kwa ushirikiano na serikali ya kaunti ya Pokot magharibi kupitia idara ya kilimo umetoa mbuzi 622 aina ya gala kwa makundi 67 ya wakulima wanaoendeleza kilimo cha ufugaji katika wadi tatu za Lomut, Endough na Alale.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mbuzi hao eneo la Nasukuta mshirikishi wa mradi huo kaunti ya Pokot magharibi Philip Ting’aa alisema mpango huo ni katika juhudi za kuimarisha shughuli za wafugaji hasa ikizingatiwa manufaa makubwa yanayoambatana na mbuzi hao.

“Aina hii ya Mbuzi wana manufaa mengi sana ikiwemo kukua kwa haraka, wana kilo nyingi na pia wanatoa maziwa mengi ikilinganishwa na mbuzi hawa wa kawaida. Kwa hivyo serikali imejitolea kuwasaidia wafugaji wa kaunti hii ili kuimarisha mapato yao.” Alisema Ting’aa.

Ting’aa alisema kwamba mradi huo ambao umegharimu kima cha shilingi milioni 22 ni moja tu ya miradi ambayo inaendeshwa na shirika hilo katika kuwawezesha wakulima pamoja na kuhakikisha usalama wa chakula, ikiwa ni pamoja na mradi wa unyunyiziaji maji mashamba.

“Mradi huu umetugharimu shilingi milioni 22 kuwaleta mbuzi hawa ili waweze kubadilisha mbuzi wetu wa hapa. Kando na huu mradi pia tunaendeleza miradi mingine ya unyunyiziaji maji mashamba ikiwemo ule wa kigen kwenye wadi ya Soak miongoni mwa mingine.” Alisema.

Kwa upande wa waziri wa kilimo kaunti hii Alfred Longronyang ambaye aliongoza ukaguzi wa mbuzi hao alisema kwamba mradi huu ni moja tu ya mikakati ya serikali kwa ushirikiano na mashirika mbali mbali kuimarisha kilimo cha ufugaji ambacho kitainua uchumi wa kaunti hii.

“Mradi huu ni moja tu ya mikakati ambayo serikali ya gavana Kachapin imeweka kwa ushirikiano na mashirika mbali mbali ili kuhakikisha kwamba wafugaji katika kaunti hii wanafaidika na kilimo hicho.” Alisema Longronyang.