VIONGOZI POKOT MAGHARIBI WATETEA MIKAKATI YA RAIS KUIMARISHA UCHUMI WA NCHI.

Baadhi ya viongozi wanaoegemea chama cha UDA katika kaunti ya Pokot magharibi wametetea uongozi wa rais William Ruto dhidi ya shutuma kutoka kwa wapinzani wake kuhusiana na kupanda gharama ya maisha nchini.

Wakiongozwa na mbunge wa Sigor Peter Lochakapong, viongozi hao walisema kwamba rais William Ruto ameweka mikakati ya kutosha kuimarisha uchumi wa taifa akiwataka wananchi kuwa na subira na kumpa nafasi ya kuhakikisha kwamba gharama ya maisha inarudi chini.

Wakati uo huo Lochakapong aliunga mkono pendekezo la rais Ruto kuwatoza wafanyikazi asilimia tatu ya mishahara kufanikisha mradi wa nyumba za bei nafuu, akisema kwamba mpango huo unalenga kuwanufaisha wakenya wenye mapato ya chini kumiliki nyumba na pia kubuni nafasi za ajira.

Aliwataka wakazi wa kaunti hii kuunga mkono mipango ya rais ili kuliendeleza mbele taifa hili.

“Tumuunge rais mkono ili aweze kuendeleza taifa mbele, kwa sababu nafahamu rais Ruto hawezi kupotosha taifa hili. Maono aliyo nayo ni ya kuendeleza taifa. Nafahamu kwamba gharama ya maisha iko juu lakini mikakati ambayo ameweka rais itapelekea gharama ya maisha kurudi chini katika kipindi cha miezi sita ijayo.” Alisema Lochakapong.

Ni kauli ambayo ilisisitizwa na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto ambaye aidha alisisitiza haja ya viongozi na wakazi wa kaunti hiyo kuunga mkono chama cha UDA ambacho chini ya muungano wa Kenya kwanza kimebuni serikali, ili kuwa katika nafasi bora ya kuafikiwa maendeleo kaunti hiyo.

“Sisi hapa ni watu wa UDA. Tukifika bungeni tunaungana na wengine na inakuwa Kenya kwanza ila hapa nyumbani ni UDA. Kwa hivyo nataka tuungane wote tuwe katika chama kimoja cha UDA ili tukiitisha maendeleo kutoka kwa serikali iwe rahisi kupata maendeleo hayo.” Alisema Moroto.