WANANCHI WATAKIWA KUZINGATIA KANUNI ZA KUHIFADHI MAZINGIRA.

Wananchi wametakiwa kuhusika kikamilifu katika kuhakikisha kwamba matumizi ya karatasi za plastiki yanapunguzwa nchini ili kukabili uchafuzi wa mazingira ambao husababishwa na karatasi hizo.

Akizungumza eneo la Chepareria kaunti hii ya Pokot magharibi wakati wa maadhimisho ya siku ya mazingira, afisa katika mamlaka ya mazingira NEMA Cliff Barkach alisema kwamba asilimia kubwa ya uchafuzi wa mazingira husababishwa na vifaa ambavyo vimetengenezwa kutokana na plastiki.

“Chanzo kikuu cha uchafuzi wa mazingira ni vifaa ambavyo vinatengenezwa kutumia plastiki. kwa hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kwamba matumizi ya karatasi za plastiki yanakabiliwa ili kupunguza uharibifu wa mazingira katika kaunti yetu.” Alisema Barkach.

Alkamai Bonface kutoka chuo kikuu cha Eldoret alitaja mbinu mbovu za ukulima, uvunaji wa mchanga usiodhibitiwa pamoja na ukataji wa miti kwa ajili ya uchomaji makaa kuwa maswala yanayochangia kuathirika mazingira akisema kwamba ipo mikakati  ambayo inaendelezwa kuangazia hali hiyo.

“Watu wengi eneo hili wamekuwa wakitaka miti sana kwa ajili ya uchomaji makaa. Na pia mbinu mbovu za ukulima zimechangia pakubwa mmomonyoko wa udongo. Kuna pia hii shughuli ya uzoaji mchanga usiodhibitiwa. Maswala haya pia yanachangia katika kuathiri mazingira.” Alisema Alkamai

Kwa upande wake naibu kamishina eneo la Kipkomo Teresia Wanjiku alisema kwa ushirikiano na wadau wengine wamebuni sheria ambayo itatumika kudhibiti shughuli ya kuvuna mchanga katika harakati za kuhakikisha kwamba shughuli hiyo inatekelezwa kwa kuzingatia utunzaji wa mazingira wakati uo huo ikiwafaidi wakazi wa eneo la Kipkomo.

“Tumebuni sheria ambayo itadhibiti uzoaji mchanga kwenye mito kwa sababu tumegundua kwamba shughuli hii inachangia katika uharibifu wa mazingira na hata wakazi wa eneo hili hawanufaiki kutokana nayo.” Alisema Wanjiku.