MIITO YAENDELEA KUTOLEWA KWA WAKAZI MPAKANI PA POKOT MAGHARIBI KUDUMISHA AMANI.
Waziri wa afya kaunti ya Pokot Magharibi Cleah Parkleah ametoa wito kwa wakazi wa kaunti hiyo na kaunti jirani ya Turkana hasa eneo la mpakani pa kaunti hizi mbili kuendelea kudumisha amani miongoni mwao.
Akizungumza katika shule ya upili ya mseto ya Turkwel Gorge wakati wa kusambaza vitambaa vya hedhi kwa wanafunzi wa kike wa shule hiyo, Parklea alisema kwamba hamna maendeleo yoyote ya muhimu ambayo yanaweza kuafikiwa iwapo hapatakuwa na amani.
Parklea alitumia fursa hiyo pia kutoa wito kwa wazazi kaunti hiyo kujitenga na tamaduni ya ukeketaji na ndoa za mapema miongoni mwa watoto wa kike, na kuwapa nafasi ya kusoma ili pia waweze kuafikia ndoto zao maishani kama wenzao wa kiume.
“Maswala ya kuwaoza watoto wetu mapema yanafaa kukoma ili tuyape masomo kipau mbele. Nashukuru pia kwamba tumeanza kushuhudia amani maeneo haya ya mpakani, na nawahimiza wakazi kuendelea kudumisha hilo kwa sababu hamna maendeleo yoyote ambayo yanaweza kuafikiwa bila amani.” Alisema Parklea.
Ni kauli ambayo ilisisitizwa na mkewe mbunge wa Likuyani Nabii Nabwera, Bi. Jacklyne Nabwera aliyehudhuria hafla hiyo miongoni mwa viongozi wengine, ambaye aliwahimiza wanafunzi kuwa msitari wa mbele katika kuhimiza amani kwa kuwahamasisha wazazi wao kuhusu umuhimu wa kuishi kwa amani na majirani.
“Naomba kupitia kwenu wanafunzi mhamasishe wazazi pale nyumbani kuhusu umuhimu wa kuishi kwa umoja na amani na majirani zetu ili tuendelee mbele. Tutumie hii fursa ambapo sasa tuna serikali za magatuzi kujiendeleza ili tufika mahali.” Alisema Bi Nabwera.