WAKAZI WA PARUA WALALAMIKIA KAZI DUNI ILIYOTEKELEZWA NA MWANAKANDARASI KATIKA BARABARA YA KOCHI HADI PARUA.
Wakazi wa eneo la Parua eneo bunge la pokot kusini katika kaunti ya Pokot magharibi wamelalamikia kazi duni ambayo imetekelezwa na mwanakandarasi aliyepewa jukumu la kukarabati barabara ya kutoka Kochi hadi parua.
Wakiongozwa na Cosmas Kiragau, wakazi hao walisema kwamba mwanakandarasi huyo alichukua muda mfupi zaidi kukamilisha shughuli ya ukarabati wa barabara hiyo bila kuzingatia taratibu zinazohitajika, na sasa wanadai hali yake ni mbovu zaidi kuliko ilivyokuwa awali hasa panaponyesha mvua.
Wamekosoa mfumo wa kupitisha maji kwenye barabara hiyo waliodai ni mbovu zaidi ikilinganishwa na fedha ambazo zilitumika katika shughuli nzima.
“Kuna mwanakandarasi ambaye alikarabati barabara ya kutoka Kochi hadi Parua. Alifanya shughuli hiyo kwa siku mbili na sasa ni mbaya kuliko jinsi ilivyokuwa awali. Mvua ikinyesha barabara hii ni tatizo kwa sababu ya mfumo mbaya wa kupitisha maji.” Walisema wakazi.
Wakazi hao sasa wanamtaka mwanakandarasi huyo kurejea eneo hilo na kuwaelezea wakazi jinsi zilivyotumika fedha za kugharamia ukarabati wa barabara hiyo hali iliyopelekea viwango duni vya kazi iliyotekelezwa.
“Tunachotaka ni huyu mwanakandarasi kurejea hapa na kutuambia jinsi pesa zilizotengewa ukarabati wa barabara hii zilizvyotumika. Kwa sababu hata vifaa vilivyotarajiwa kutumika katika barabara hii havikutumika.” Walisema.