6 wakamatwa Tambalal, Pokot magharibi kufuatia mzozo wa ardhi

Gari la Polisi Likisafirisha Watu waliokamatwa Tambalal Kamatira,Picha/Benson Aswani

Na Emmanuel Oyasi,
Taharuki imetanda katika kijiji cha Tambalal eneo la Kamatira, Kaunti Ndogo ya Kipkomo katika Kaunti ya Pokot Magharibi baada ya zaidi ya watu sita kukamatwa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika kile kinachoaminika kuwa mzozo wa ardhi.


Mzozo huo wa miaka 50 umearifiwa kuzidishwa na hatua ya maafisa wa polisi kuwakamata wakazi wanaodai kumiliki ardhi hiyo kwa miongo kadhaa sasa.


Mzozo huo unaohusu ardhi ya zaidi ya ekari 100 na ambao unahusisha pande mbili umewaacha wakazi wengi kulala kwenye kibaridi katika eneo la Kamatira kando ya barabara kuu ya Kitale Lodwar baada ya polisi kuvamia kijiji hicho siku ya Jumamosi.


Kulingana na maelezo ya mahakama, kesi hiyo iliamuliwa miaka 5 iliyopita, hata hivyo wiki iliyopita mahakama kuu ya Kitale iliamuru kwamba wote wanaomiliki ardhi hiyo wafurushwe.
Familia zilizoathirika sasa zinaiomba serikali ya kaunti na kitaifa kuingilia kati suala hilo na kuwapa misaada ya kibinadamu.


“Tunahangaika sana huku, hatuna pa kwenda kwa sababu kwa miaka mingi tumepajua mahali hapa kuwa nyumbani kwetu. Tunaomba tu serikali kuingilia kati na kutusaidia kupata haki yetu,” alisema mmoja wa familia hizo.


Aliyekuwa mwakilishi wadi Teresa Lokichu ambaye ni mzawa wa kijiji hicho ametoa wito wa haki kwa watu walioathirika na kuongeza kuwa Serikali inapaswa sasa kutoa ardhi mbadala kwa waathiriwa hao
Alisema wamekata rufaa dhidi ya kesi hiyo na wakaazi hawapaswi kufukuzwa.


“Ni kama hawa watu wa Tambalal hawana haki, na ni watu walizaliwa hapa. Ningeomba hii iwe ya mwisho. Wasikuje tena kuwahangaisha wakazi. Tumekata rufaa na hawa polisi wanafaa kusubiri hadi hiyo kesi isikilizwe,” alisema Lokichu.


OCPD wa Kipkomo Njoroge Mbugua alithibitisha kuwa watu sita wamekamatwa akisema kulikuwa na hati ya kukamatwa kwa watu 13 ambao Mahakama ya Kilimo ya Kitale iliwaagiza kufika mbele yake tarehe 12 Machi 2025.