WAKAAZI ZAIDI YA 600 KUTOKA CHEPCHOINA WAKOSA MAKAAZI BAADA YA MVUTANO KUIBUKA BAINA YAO NA MAAFISA WA JESHI


Mvutano baina ya wakazi wa Chepchoina na maafisa wa Jeshi umezuka kwa mara nyingine huku wakazi zaidi ya 600 wakikosa mahali pa kuishi baada ya jeshi hilo kubomoa nyumba zao wakiwataka wahame kutoka kwa mashamba ya serikali.
Ni kisa ambacho kimeshtumiwa vikali na seneta wa kaunti ya Pokot Magharibi Daktari Samuel Poghisio ambaye amewaonya vikali maafisa wa serikali wanaohusika kwenye ubomozi bila idhini yoyote kutoka kotini.
Hata hivyo Poghisio amesema suluhisho kamili litaafikiwa tu iwapo serikali itawapa wakazi hao hatimiliki ya mashamba hayo.
Mbunge wa Kapenguria Samuel Moroto kwa upande wake amesema wakazi wa Chepchoina wana idhini kamili ya kuishi humo kutoka kortini japo kumekuwapo na suala la kisiasa tangu hayati Rais Daniel Moi alipokuwa uongozini.
Amesema mashamba hayo yalipeanwa kwa wananchi kutoka kwenye jamii mbalimbali nchini ikiwa ni njia mojawapo za kudumisha amani na utangamano baina ya jamii zinazoishi mpakani humo.