Yanga ndio mabingwa wa ligi kuu nchini Tanzania wa mwaka 2024/2025

NA PRESENTER WAKOLI
Ligi kuu ya Tanzania bara msimu wa 2024/25 imehitimishwa kwa namna isiyo ya kawaida. Yanga SC, klabu yenye historia kubwa na ushawishi mpana katika soka la Tanzania, imetwaa ubingwa wake wa nne mfululizo na wa 31 kwa jumla, baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya mahasimu wao Simba SC katika mchezo wa mwisho wa msimu uliofanyika Juni 25, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kwa kawaida, ubingwa huleta shamrashamra, sherehe na maadhimisho. Lakini msimu huu, hisia hizo zimepungua kwa kiasi fulani, huku ligi ikimalizika katika mazingira ya sintofahamu, maswali mengi yasiyojibiwa, na kumbukumbu ya mvutano uliohusisha siasa, ushawishi, na sintofahamu ya kiutawala.
Kilichoanza kama sakata la kuahirishwa kwa mechi moja, ile ya dabi ya Kariakoo iliyokuwa ichezwe Machi 8, 2025 kimegeuka kuwa doa kubwa katika uhalali na taswira ya ligi nzima. Mechi hiyo, iliyowekwa kwa ajili ya kuamua mwelekeo wa ubingwa, iliahirishwa kwa mazingira yasiyoeleweka, na ikachezwa takribani miezi minne baadaye.
Licha ya kufungwa kwa pazia rasmi, maswali muhimu yamebaki hewani hasa kuzungumza mchezo wa dabi namba 184. Haya si maswali ya kawaida tu ya soka, bali ni maswali yanayozunguka mamlaka, maamuzi, uwajibikaji, na uadilifu wa taasisi zinazosimamia mchezo huu pendwa.