Wachezaji Amos Wanjala na Aldrine Kibet wanaelekea kucheza nchini Uhispania

Nahodha wa timu ya taifa ya wachezaji wa chini ya umri wa miaka 20, Amos Wanjala, anatarajiwa kusaini mkataba na klabu ya Elche CF nchini Uhispania, akijiunga na mwenzake Aldrine Kibet katika hatua kubwa kuelekea ligi ya juu ya LaLiga.

Uhamisho wa Wanjala hadi Elche CF unatarajiwa kukamilika hivi karibuni, hatua inayochukuliwa kuwa muhimu sana katika taaluma yake ya soka.

Wakati huo huo, Aldrine Kibet pia anatarajiwa kujiunga na klabu ya Celta Vigo. Kibet, ambaye pia ni mchezaji mahiri wa timu ya U20, tayari ana wazazi wake nchini Uhispania kwa maandalizi ya mwisho ya uhamisho wake.

Waziri wa zamani wa Michezo, Ababu Namwamba, amekuwa miongoni mwa watu waliounga mkono kwa dhati maendeleo ya wachezaji hao, akiwa na mchango mkubwa katika kuwawezesha kujiunga na Chuo cha Soka cha Nastic nchini Uhispania.

Namwamba alieleza fahari yake kwa mafanikio ya Wanjala na Kibet, akisisitiza kuwa mafanikio yao ni hatua muhimu kwa maendeleo ya soka nchini Kenya.

“Hongera sana vijana wangu Aldrine Kibet na Amos Wanjala kwa hatua hii kubwa kuelekea ligi ya kifahari ya LaLiga, Tuliota ndoto kubwa, tuliamini, sasa imekuwa kweli!”

Wachezaji Kibet na Wanjala walijipatia umaarufu kitaifa baada ya kuonyesha uwezo wa hali ya juu na kujituma kwao kulikoiwezesha Shule ya Wavulana ya St. Anthony’s, Kitale kutwaa taji la michezo ya kitaifa ya shule za upili mwaka 2023.

Maendeleo haya ni hatua muhimu siyo tu katika taaluma zao binafsi, bali pia katika historia pana ya ustawi wa soka la Kenya.

“Kwa wale waliokuwa na mashaka au waliouliza kuhusu Talanta Hela, haya ndiyo matunda ya maono mapya. Tambua. Kuza. Faidi—tukitekeleza kwa njia ya makusudi na iliyoratibiwa. Kutoka mashindano ya shule, kupitia Kenya Academy of Sports, hadi Nastic Soccer Academy huko Tarragona, na sasa hadi katika soka la kulipwa la daraja la juu.” Alisema Namwamba