Mchezaji wa Arsenal alazwa hospitalini baada kudungwa kisu na mwendawazimu

•Mari alikuwa miongoni mwa watu sita ambao walishambuliwa kwa kisu na mwendawazimu mmoja kwenye jumba la maduka katika jiji la Milan jana jioni.

•Arsenal ilituma ujumbe wake wa faraja kwa Pablo na wahasiriwa wengine watano wa tukio hilo la kuogofya. Klabu ya soka ya Arsenal imemtakia afueni ya haraka beki wake Pablo Mari baada ya kushambuliwa Alhamisi jioni.

Mari ambaye yuko kwa mkopo katika klabu ya Italia, A.C Monza alikuwa miongoni mwa watu sita ambao walishambuliwa kwa kisu na mwendawazimu mmoja kwenye jumba la maduka katika jiji la Milan jana jioni.

Ripoti kutoka Italia na klabu ya Arsenal zinadokeza kuwa mwanasoka huyo wa Uhispania kwa sasa anaendelea kupata nafuu hospitalini. Mari hata hivyo yuko nje ya hatari kwani alipata majeraha madogo tu.

“Sote tumeshtushwa kusikia habari mbaya kuhusu tukio la kuchomwa visu nchini Italia, ambalo limewaweka watu kadhaa hospitalini akiwemo beki wetu wa kati anayecheza kwa mkopo Pablo Mari. Tumekuwa tukiwasiliana na ajenti wa Pablo ambaye ametuambia yuko hospitalini na hajaumia sana,” Arsenal ilisema katika taarifa. Shambulizi hilo lilijiri jioni ambapo Wanabunduki walipata kichapo cha aibu dhidi ya PSV  ya Uholanzi katika mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Europa. PSV ilipiga Arsenal 2-0 katika mechi ya mkondo wa pili.