Hazina ya michezo inafaa kufadhili michezo pekee; Mvuria

Salim Mvuria waziri wa michezo na maswala ya vijana kenya, Picha/Maktaba

Na Emmanuel Oyasi,
Serikali imeanza kuchukua hatua za kulinda mfuko wa michezo, sanaa na maendeleo ya jamii wito ukitolewa wa kufanyiwa marekebisho ya sheria ili kuhakikisha kwamba mfuko huo unatumika kikamilifu katika maswala yanayohusu michezo.


Akizungumza katika kikao cha pamoja na kamati ya kitaifa kuhusu michezo na utamaduni, waziri wa michezo Salim Mvuria aliwafahamisha wabunge kuhusu utendakazi wa hazina hiyo na hitaji linaloongezeka la kurahisisha matumizi yake.


“Kwa sasa hazina ya michezo inafadhili shughuli nyingi za michezo kote nchini, na hii ndio maana tunatafuta vyanzo tofauti vya fedha ili tufanikishe Nyanja mbali mbali katika sekta ya michezo,” alisema Mvuria.


Aidha Mvuria alisisitiza haja ya kukagua kanuni zilizopo na uwezekano wa kuanzisha sheria mpya inayofafanua waziwazi kile ambacho hazina hiyo inapasa kugharamia.


Alibainisha kwamba mashauriano yanaendelea na mwanasheria mkuu wa serikali na hazina ya kitaifa ili kuunda muundo thabiti wa kisheria ambao utasimamia hazina hiyo.


“tunaangazia upya kanuni zilizopo, na jinsi ya kuhakikisha kwamba hazina ya michezo inaelekezwa kwa maswala maalum. Lakini ilivyo kwa sasa maneno yote unayosikia ya michezo ya kuigiza katika idara ya elimu ni hazina ya michezo inayofadhili,” alisema.