Chekeruk alalamikia kutengwa eneo la Masol Kimaendeleo

Mwakilishi wadi wa Masol Wilson Chekeruk akihutubia wakaazi wa eneo la Masol, Picha/Benson Aswani

Na Benson Aswani,
Mwakilishi wadi ya Masol eneo bunge la Sigor katika kaunti ya Pokot magharibi Wilson Chekeruk amelalamikia kile amedai kutengwa pakubwa wakazi wa eneo hilo katika huduma mbali mbali muhimu za serikali.


Katika mahojiano na kituo hiki, Chekeruk alisema ikilinganishwa na maeneo mengine nchini, eneo la Masol limesalia nyuma pakubwa kutokana na ukosefu wa huduma kama vile umeme, vituo vya afya pamoja na maji safi ya matumizi miongoni mwa huduma nyingine muhimu.


Chekeruk sasa anatoa wito kwa serikali kupitia idara husika kuhakikisha kwamba wakazi wa eneo hilo pia wanafikia na huduma hizo muhimu ili kuwapa fursa pia ya kuafikia maendeleo kama ilivyo katika maeneo mengine ya nchi.


“Hatuna umeme katika wadi nzima ya Masol. Tunaomba serikaIi kuhakikisha umeme unafika katika wadi hii ili tuwe sawa na maeneo mengine ya nchi. Pia hatupokei huduma muhimu maeneo haya kama vile maji safi na huduma za afya kwa kuwa hatuna hospitali,” alisema Chekeruk.


Wakati uo huo Chekeruk alilalamikia idadi kubwa ya wakazi ambao hawana vitambulisho vya kitaifa eneo hilo la Masol, hali ambayo pia inachangia kwao kupitia wakati mgumu wanapotafuta huduma muhimu za serikali.


“Tuna wakazi wengi katika wadi hii lakini sasa idadi kubwa ya wakazi hawa hawana vitambulishi vya kitaifa, hali ambayo inawapelekea kupitia wakati mgumu wanapotafuta huduma muhimu za serikali,” alisema.