Ni sisi wenyewe tunaolemaza soka ya humu nchini; Kachapin

Simon Kachapin Gavana wa kaunti ya pokot magharibi, Picha/Maktaba
Na Emmanuel Oyasi,
Mwenyekiti wa kamati ya michezo katika baraza la magavana Simon Kachapin amesema mchezo wa kandanda hapa nchini haujafikia viwango vya kuridhisha ikilinganishwa na mataifa mengine barani Afrika kutokana na kutopata uungwaji mkono unaohitajika.
Kachapin ambaye pia ni gavana wa kaunti ya Pokot magharibi amesema hali kwamba wengi wa wakenya wameelekeza ushabiki wao katika klabu za mataifa ya ughaibuni hasa ligi kuu ya uingereza na kutoonyesha nia ya kuunga mkono soka ya hapa nchini, inalemaza juhudi za kuimarisha soka.
Gavana Kachapin amesema taifa hili lina wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kulifanya kuwa miongoni mwa mataifa yaliyobobea katika soka, iwapo tu watapata uungwaji mkono mkamilifu.
“Wale wanaopenda Manchester United, Arsenal au Chelsea, hao ni Eurocentric minded people, na hiyo haitajenga Afrika kwa sababu tunafaa kuunga mkono timu zetu. Tukiwa na mawazo kwamba kila jioni tunashabikia soka ya nje, kenya hii haitafika mahali,” alisema Gavana Kachapin.
Kachapin alisema hali kwamba taifa hili halijawahi kuwakilishwa katika michuano ya kombe la dunia ni ishara tosha ya jinsi mchezo wa soka haudhaminiwi nchini.
“Ningependa sana soka ya hapa nchini inawiri. Hali kwamba hatujawahi kuwakilishwa katika michuano ya kombe la dunia tangu kuumbwa dunia, inaamanisha kwamba hatujipendi wenyewe,” alisema.